Bei mpya za mafuta zilizotangazwa Oktoba 7, 2026, zimeendelea kuifanya Tanzania kuwa na bei himilivu na nafuu za mafuta ikilinganishwa na nchi nyingi jirani na za mbali, licha ya sekeseke la mgogoro wa Mashariki ya Kati unaochochea kupanda kwa bei za mafuta na kusababisha misukosuko mikubwa katika soko la nishati duniani.
Kwa mujibu wa takwimu za ulinganisho wa bei za mafuta, petroli nchini Tanzania inauzwa Sh 4,057 kwa lita, ikiwa chini ya Malawi yenye Sh 8,466, Zimbabwe Sh 5,435, Rwanda Sh 5,251, Uganda Sh 4,815, Kenya Sh 4,360, Namibia Sh 4,342 na Zambia Sh 4,211.
Kwa upande wa dizeli, Tanzania ina bei ya Sh 4,086 kwa lita, ikiwa chini ya Malawi yenye Sh 8,834, Zimbabwe Sh 5,487, Rwanda Sh 5,232, Mozambique Sh 4,753, Uganda Sh 4,675, Namibia Sh 4,553, Zambia Sh 4,453 na Kenya Sh 4,438.
Katika nchi za mbali, ulinganisho wa bei za petroli unaonesha Ujerumani ikiwa na bei ya takribani Dola 2.35 sawa na Sh 6,190 kwa lita, Ufaransa Dola 2.49 sawa na Sh 6,559, Uholanzi Dola 2.76 sawa na Sh 7,270 na Denmark Dola 2.97 sawa na Sh 7,823.
Nchini Singapore, bei ya petroli imefikia takribani Dola 2.76 sawa na Sh 7,270 kwa lita, huku dizeli ikiuzwa Dola 3.13 sawa na Sh 8,244 kwa lita.
Kwa upande wa Uingereza, bei ya dizeli imefikia Dola 2.64 sawa na Sh 6,954 kwa lita, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko bei ya Sh 4,086 inayotumika Tanzania.
Tofauti hizo zinaonesha kuwa Tanzania inaendelea kuwa na bei nafuu za mafuta ikilinganishwa na nchi nyingi za Afrika, Ulaya na Asia, wakati mgogoro wa Mashariki ya Kati ukiendelea kuweka shinikizo katika uzalishaji, usafirishaji na biashara ya mafuta duniani.
Hadi Oktoba 7, Tanzania, Zambia na Namibia ndizo nchi zilizokuwa zimetangaza bei mpya za mafuta kwa mwezi Oktoba, huku bei ya dizeli nchini Namibia ikiwa haijabadilika.
