You are currently viewing BEI YA MAFUTA GHAFI HAISHIKIKI DUNIANI TANGU AGOSTI

BEI YA MAFUTA GHAFI HAISHIKIKI DUNIANI TANGU AGOSTI

MGOGORO wa Mashariki ya Kati umeifanya dunia kuendelea kuonja joto la jiwe, baada ya bei ya mafuta ghafi aina ya Brent kuendelea kuwa juu tangu Agosti, kutoka wastani wa dola 91 kwa pipa mwezi huo hadi kuvuka dola 100 Septemba na kuendelea kuzunguka kiwango hicho mwanzoni mwa Oktoba, hali iliyopelekea bei za mafuta katika nchi mbalimbali kuendelea kuwa juu.

Petroli imefikia takribani Sh8,462 kwa lita Malawi, Sh7,441 Denmark, Sh7,236 Netherlands, Sh6,066 Uingereza, Sh5,433 Zimbabwe, Sh5,239 Rwanda, Sh4,499 Uganda, Sh4,347 Kenya na Sh4,194 Afrika Kusini, huku Tanzania ikiwa Sh3,796 na Zambia Sh3,377 huku nchini Marekani imefikia karibu Sh16,850 kwa gallon, kutoka Sh12,200 kabla ya mgogoro, ongezeko la takribani asilimia 38.

Tanzania na nchi nyingine zinazoagiza mafuta sasa zinakabiliwa na mabadiliko ya bei katika mwezi huu wa Oktoba, wakati mafuta yaliyonunuliwa katika kipindi ambacho bei ya mafuta ghafi ilikuwa juu yakianza kuingia katika masoko yao.

Tanzania hadi sasa imeendelea kuhimili shinikizo hilo, petroli Dar es Salaam ikiwa Sh3,796 kwa lita, chini ya Sh3,898 ya Agosti na Sh3,990 ya Julai, lakini bei kubwa ya mafuta ghafi ya Agosti na Septemba inaweka shinikizo jipya katika bei za Oktoba na miezi inayofuata.

Ifahamike kuws mgogoro wa Mashariki ya Kati na hofu ya kuvurugika kwa uzalishaji na usafirishaji kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz vimeendelea kuweka soko la mafuta duniani katika presha ambapo njia hiyo ni miongoni mwa mishipa muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani, huku hatari ya usalama ikiongeza pia gharama za meli na bima na kufanya mafuta yanayofikishwa katika nchi zinazoagiza kuwa ghali zaidi.

Leave a Reply