You are currently viewing WIZARA YA MAJI KUIMARISHA USTAWI WA WATUMISHI – AWESO

WIZARA YA MAJI KUIMARISHA USTAWI WA WATUMISHI – AWESO

Na Mwandishi wetu

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amesema Wizara ya Maji itaendelea kushirikiana na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) ili kuimarisha ustawi na maendeleo ya watumishi wa Sekta ya Maji.

Akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo katika Kikao cha Pili cha Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika katika Mji wa Serikali – Mtumba, jijini Dodoma, Aweso amesisitiza kuwa watumishi ndio mhimili mkuu wa mafanikio ya sekta hiyo na kutambua mchango wao mkubwa katika kufanikisha malengo ya Wizara.

Ameeleza kuwa Wizara inathamini mchango wa watumishi wake na itaendelea kuchukua hatua za kusimamia haki zao za msingi, ikiwemo ustawi na maendeleo yao. Amebainisha kuwa ushirikiano na TUGHE utaimarishwa katika ngazi zote za tawi, mkoa na taifa kwa lengo la kulinda maslahi ya watumishi wa Sekta ya Maji.

“Wizara ya Maji ina watumishi wenye uwezo mkubwa, jambo linalotusaidia kufikia malengo yetu ya kisekta. Sisi viongozi tutaendelea kusimamia haki zenu za msingi, ikiwemo ustawi na maendeleo yenu,” Aweso amesema.

Aidha, Waziri Aweso amewataka watumishi kuzingatia nidhamu ya kazi kwa kujituma na kujitoa kikamilifu, badala ya kufanya kazi kwa woga. Pia, amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji katika maeneo yote ya kazi ili kuongeza ufanisi na tija.

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa watumishi wote bila kujali kada au vyeo, akibainisha kuwa kutoa nafasi kwa kila mmoja kutoa maoni ni msingi wa mafanikio ya sekta. Ameongeza kuwa Wizara itaendelea kutoa motisha na kutambua watumishi wanaofanya kazi kwa bidii, pamoja na kuboresha mazingira ya kazi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amemshukuru Waziri Aweso na watumishi wote kwa ushirikiano wao katika kufanikisha malengo ya taasisi.
“Mafanikio tuliyoyapata katika utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025 ni kielelezo cha umoja na mshikamano wetu. Huu ndio msingi mkuu wa mafanikio yetu,” Mhandisi Mwajuma amesema.

Aidha, alieleza kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali, Menejimenti ya Wizara inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuzitatua kwa manufaa ya watumishi na taasisi kwa ujumla.